You Are Here: Home » Whats New » DKT. NDUMBARO AWATAKA WALIOVAMIA MAENEO YA HIFADHI KUONDOKA

DKT. NDUMBARO AWATAKA WALIOVAMIA MAENEO YA HIFADHI KUONDOKA

DKT. NDUMBARO AWATAKA WALIOVAMIA MAENEO YA HIFADHI KUONDOKA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro leo Jumamosi tarehe 1Januari, 2021 ameongoza doria ya kuangalia hali ya uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Pori la Akiba la Gesimasowe pamoja na Litumbandosi na kutoa agizo kwa Wavamizi walioanzisha shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo kinyume cha Sheria waanze kuondoka wenyewe.

Doria hiyo iliyofanyika kwa kutumia ndege ndogo mali ya Shirika la Hifadhi za Taifa ( TANAPA)  imeshuhudia uharibifu mkubwa unaotokana na shughuli za kibindamu.

Katika doria hiyo Dkt.Ndumbaro amejionea makundi makubwa ya mifugo pamoja nyumba za kudumu zilizojengwa ndani ya  maeneo ya  Hifadhi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Akizungumza mara baada ya doria hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Damas Ndumbaro amewataka Wafugaji na Wakulima nchi nzima ambao wanaendesha shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo ya hifadhi waanze kuondoka wenyewe kabla Operesheni ya kuwaondoa haijaanza.

” Kama mnanisikia anzeni kuondoka wenyewe kabla hatujawabaini tutakamata mifugo na mtalipa gharama zote za kuharibu mazingira” amesisitiza Dkt.Ndumbaro

Amesema kwa mujibu wa sheria maeneo hayo yametengwa kwa ajili ya shughuli za uhifadhi pekee na yeyote anayetaka kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo anarudisha nyuma juhudi za uhifadhi nchini

“Katika kipindi changu cha uongozi sitakubali kuona uhifadhi unachezewa kwa sababu maeneo haya ni kichocheo cha Uchumi wa Taifa letu kupitia shughuli za utalii ikiwemo  utalii wa picha na uwindaji wa kitalii ambapo kupitia utalii nchi imekuwa ikipata fedha nyingi.” Amesema Dkt. Ndumbaro.

Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro ameziagiza Taasisi za Uhifadhi nchini zikamate mifugo itakayokutwa Hifadhini bila kujali mifugo hiyo inamilikiwa na nani

” Nawaagize hata mkiikuta mifugo yangu, ninyi kamateni, msiogope kamateni tu ” amesisitiza Dkt. ndumbaro.

© 2021 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top