You Are Here: Home » Whats New » WANANCHI SONGWE WATAKIWA KUACHA KUVAMIA MAENEO YA HIFADHI

WANANCHI SONGWE WATAKIWA KUACHA KUVAMIA MAENEO YA HIFADHI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewaasa wananchi wa Kitongoji cha Nkanka ,Kijiji cha Itumba katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe, kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi hasa katika eneo la Hifadhi ya Msitu wa Ileje Range.

Amesema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ya Kutatua migogoro ya ardhi wilayani humo.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhia Kitongoji cha Nkanka kirasimishwe ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Ileje Range, na kuwataka wananchi kuacha kuendelea kumega eneo la msitu huo kwa ajili ya matumizi yao binafsi.

“Sasa niwaombe huruma ya Mheshimiwa Rais isije ikawafanya mkajisahau, ninyi sasa hivi mtakuwa sehemu ya hifadhi mtasimamia na kuhakikisha miti haichomwi, haikatwi hovyo na shughuli za kibinadamu haziingii kwenye eneo hili la hifadhi” amesisitiza.

Amesema ni lazima kulihifadhi eneo hilo na kulisimamia lisiingiliane na shughuli za kibinadamu ili kutunza mazingira na kuepukana na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayopelekea kuwepo kwa ukame.
Amefafanua kuwa baada ya wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na wajumbe wa Nkanka, kufanya marudio ya kutambua na kuweka vigingi wananchi hawataruhusiwa kuingia tena ndani ya hifadhi hiyo.

Amewataka wananchi hao kusimamia vizuri eneo watakalopewa kwa kupanga matumizi bora ya ardhi na kufanya shughuli zao za kilimo na ufugaji katika eneo hilohilo.

Awali akizungumza na watendaji wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Masanja amewaomba kuendelea kutatua migogoro ya mipaka na uvamizi wa maeneo ya hifadhi ili kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutekeleza majukumu mengine ya kitaifa.

 

© 2022 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top