You Are Here: Home » Whats New » WANANCHI IRINGA WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUDHIBITI MOTO KWENYE MASHAMBA YA MITI

WANANCHI IRINGA WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUDHIBITI MOTO KWENYE MASHAMBA YA MITI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe.Mary Masanja(Mb) amewataka wananchi Mkoani Iringa kushirikiana katika kudhibiti matukio ya moto yanayojitokeza kwenye mashamba ya miti binafsi na ya Serikali.

Ameyasema hayo leo katika Kijiji cha Kibengu Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta katika Shamba la Miti Saohill.

“Niwaombe sana kila mtu awe mlinzi wa mwenzake, kama unaandaa shamba hakikisha unaangalia upepo unaelekea wapi ndipo uchome” amesisitiza.

Amewaomba wananchi kuwasiliana na viongozi wa mashamba inapofikia wakati wa kuandaa mashamba yao ili waweze kuwa karibu kudhibiti moto ambao unaweza ukajitokeza .

Amefafanua kuwa mashamba ya miti yamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kutoa ajira akitolea mfano wa Shamba la Miti Sao Hill ambalo limekuwa likitoa ajira zaidi ya 4000 kwa wananchi.

Amesema Shamba hilo pia limekuwa likisaidia katika huduma mbalimbali kwa jamii kama kusaidia ujenzi wa madarasa,zahanati, vituo vya afya pamoja na ujenzi wa shule

Aidha, shamba hilo pia huzalisha Miche ya miti ipatayo milioni 7 kila mwaka ambayo hupandwa kwenye maeneo yaliyovunwa , huwagawia wananchi na Taasisi mbalimbali binafsi.
Ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta inaendelea mkoani Njombe Oktoba 25, 2022

© 2022 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top