You Are Here: Home » Whats New » Uzinduzi wa Siku ya Taifa ya Kutundika Mizinga Tarehe 4 Machi 2013

Uzinduzi wa Siku ya Taifa ya Kutundika Mizinga Tarehe 4 Machi 2013

Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Siku ya Taifa ya Kutundika Mizinga ambayo itazinduliwa kwa mara ya kwanza Machi 4 Mwaka huu mkoani Singida katika Hifadhi ya Aghondi, iliyoko katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

TAARIFA KWA UMMA

UZINDUZI WA SIKU YA TAIFA YA KUTUNDIKA MIZINGA

TAREHE 4 MACHI 2013

Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Siku ya Taifa ya Kutundika Mizinga ambayo itazinduliwa kwa mara ya kwanza Machi 4 Mwaka huu  mkoani Singida katika Hifadhi ya Aghondi, iliyoko katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Madhumuni ya siku hiyo ambayo itakuwa inaadhimishwa kila mwaka ni kuwahamasisha wananchi kushiriki kwa wingi katika shughuli za ufugaji nyuki kwa kutumia mbinu za kisasa.

Wizara itatumia Siku ya Kutundika Mizinga kuonyesha kwa vitendo shughuli za ufugaji nyuki, kama vile kuandaa maeneo mapya ya ufugaji nyuki, kutayarisha mizinga ya nyuki, kutafuta makundi ya nyuki kwa ajili ya kuhamishia kwenye mizinga ya kisasa na kutayarisha vifaa vya ufugaji nyuki. Aidha vipeperushi vitakavyoelimisha kuhusu ufugaji nyuki wa kisasa vitaandaliwa na kutawanywa kwa wananchi.

Siku ya Kutundika Mizinga kitaifa pia itatumika kuzihamasisha Asasi mbalimbali kuwasaidia wafugaji nyuki ili waweze kufuga nyuki kwa kutumia mbinu za kisasa kwa nia ya kuzalisha mazao ya nyuki maradufu.

Vilevile wananchi watahimizwa kuanzisha vyama vya ufugaji nyuki ili kuboresha shughuli zao na kuharakisha mawasiliano kati yao na masoko.

Aidha, katika Siku ya Kutundika Mizinga elimu itatolewa kuhusu kalenda ya mwaka ya ufugaji nyuki nchini na umuhimu wa kuizingatia wakati wa kufanya shughuli za ufugaji nyuki katika maeneo mbalimbali husika.

[MWISHO]

George Matiko

MSEMAJI

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

25 Februari 2013

Simu: 0784 468047

© 2021 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top