You Are Here: Home » Whats New » TAWA YAKUTANA NA WAMILIKI WA BUCHA ZA NYAMAPORI

TAWA YAKUTANA NA WAMILIKI WA BUCHA ZA NYAMAPORI

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Jana tarehe 27/01/2021 katika ukumbi wa Malihai Club uliopo Njiro Jijini Arusha ilifanya Warsha na wamiliki wa Mabucha ya nyamapori waliokidhi vigezo vya usajili na kupewa leseni za biashara ya Nyamapori waliotoka sehemu mbalimbali nchini.


Naibu Kamishna wa Utalii Huduma za Biashara Bw. Imani R. Nkuwi akifungua Warsha hiyo alisema Lengo la Warsha ni kujadili mikakati mbalimbali ya kuwezesha biashara za bucha za Wanyamapori ili iweze kushamiri Kama matarajio ya wananchi wa Tanzania yalivyo Sasa.

Aidha, Warsha hiyo ililenga kujenga uelewa wa pamoja wa biashara hiyo kwa kuangalia tasnia nzima ya biashara,  changamoto na namna Bora ya kuboresha biashara hiyo ili iwe endelevu.

Afisa Wanyamapori - Sera na Mipango kutoka TAWA Bw. Rajabu Hochi alitoa wasilisho ambapo alielezea hali halisi ya biashara ya nyamapori, changamoto na utatuzi wake, na kutoa fursa kwa upande wa wamiliki wa mabucha kueleza changamoto wanazopitia katika kuendesha biashara hii ya nyamapori.

Changamoto kuu zilizobainishwa na wadau hao ni Kama ifautavyo:-

-Maeneo machache kwaajili ya Uwindaji wa wenyeji na uhaba wa Wanyamapori katika maeneo hayo.

-Uchache wa mgao wa Wanyamapori ( Quota) katika maeneo ya uwindaji wa wenyeji.

Akijibu baadhi ya changamoto za wamiliki hao wa Mabucha Naibu Kamishna wa Utalii Huduma za Biashara Bw. Imani Nkuwi alisema TAWA Ina mpango wa kuongeza maeneo ya Uwindaji wa wenyeji kutoka manane mpaka 20, na tayari andiko la kuomba kuongeza vitalu hivyo liko kwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Pia Naibu Kamishna huyo aliwaasa wamiliki wa mabucha kuwa ili biashara hiyo iwe endelevu ni lazima wajikite zaidi katika zoezi la kuanzisha mashamba ya Wanyamapori Kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

© 2021 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top