You Are Here: Home » Whats New » TAASISI ZA UHIFADHI ZAAGIZWA KUBORESHA MAONESHO TANGA

TAASISI ZA UHIFADHI ZAAGIZWA KUBORESHA MAONESHO TANGA

Taasisi za Uhifadhi nchini zimeagizwa kujenga mabanda ya kudumu kwenye uwanja wa maonesho ya Biashara na Utalii katika mkoa wa Tanga ili kuyapa hadhi ya maonesho hayo badala ya kuwa na mabanda ya muda mfupi.

Pia, Amezitaka Taasisi hizo na Idara za Wizara kuhakikisha kuwa zinashiriki kwenye maonesho hayo kila mwaka kutokana na mchango mkubwa wa maonesho hayo katika kuendeleza na kukuza biashara na utalii katika Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.


Akizungumza wakati akifunga maonesho ya 7 ya Biashara na Utalii mkoani Tanga, Mhe.Kanyasu amesema maonesho hayo ni fursa ya kutangaza na kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.


Mhe. Kanyasu amezitaja Taasisi hizo zinazotakiwa kushiriki kwenye maonesho hayo kuwa ni Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA) Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania-(TAWA) Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro(NCAA)  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Makumbusho ya Taifa na Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB)

Mbali na hizo, Mhe. Kanyasu amezitaka Idara za msingi za Wizara ya Maliasili na Utalii nazo kushiriki katika maonesho hayo ili kuwaelimisha wananchi kuhusiana na shughuli za Utalii, Misitu, Wanyamapori na Mambokale.

Amesema kitendo cha baadhi ya Taasisi za Uhifadhi na Idara husika kushindwa kushiriki kwenye naonesho hayo ni kuwanyima fursa wananchi kufahamu vivutio vya Utalii vilivyopo pamoja na maliasili zao

Amesema mwaka ujao wa 2020 hategemei kuona TAWA na TANAPA zikishiriki pekee kama ilivyotokea kwa mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewataka wananchi wa Tanga ambao waliokuwa wakiendesha maisha yao kwa kusafirisha baadhi ya wanyamapori hai ikiwemo vipepeo wabuni mbinu zingine za kibiashara ili kuwavutia watalii kuja nchini kuona wanyama hao badala ya kuwapelekea huko waliko.

Amesema msimamo wa Serikali upo pale pale wa kuhakikisha utalii unalindwa kwa kuhakikisha hakuna wanyamapori wanaosafirishwa kupelekwa nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Tanga Mhe.Martin Shigela amesema mkoa wa Tanga umejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ambavyo kupitia maonesho hayo kama vitaweza kujulikana kwa watu wengi na hivyo kuchagiza maendeleo kwa mkoa na Taifa kwa ujumla.

Amesema mkoa wa Tanga una vivutio vya utalii yakiwamo mapango ya Amboni pamoja na magofu ya kale pamoja na Utalii wa fukwe ambavyo vikitangazwa ipasavyo vitaweza kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea mkoa huo

© 2020 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top