You Are Here: Home » Whats New » TAARIFA KWA UMMA

TAARIFA KWA UMMA

RIPOTI YA UTAFITI WA WATALII WALIOONDOKA NCHINI MWAKA 2021


Ndugu Wanahabari

Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwenu kwa kuitikia wito huu na ushirikiano ambao mmeendelea kuutoa katika kukuza na kuendeleza Sekta ya Utalii nchini. Ni dhahiri kuwa vyombo vya habari vimekuwa mabalozi wetu wazuri katika kutoa taarifa kwa umma ikiwemo kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi.

Ndugu Wanahabari

Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa dunia. Takwimu zinaonesha kuwa kabla ya mlipuko wa janga la UVIKO-19, idadi ya watalii duniani iliongezeka kwa takribani asilimia tano.  Aidha Utalii duniani ulichangia asilimia 6.8 ya mauzo ya nje, na kuzalisha ajira milioni 333 sawa na uwiano wa ajira moja (1) kwa kila ajira nne (4) mpya duniani.

Kwa upande wa Tanzania, mwaka mmoja baada ya mlipuko wa janga la UVIKO-19, sekta ya utalii imeanza kuimarika kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na Sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii na hivyo kufanya idadi ya watalii kuongezeka hadi kufikia watalii 922,692 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka 2020. 


Ndugu Wanahabari

Mwaka 2021, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar na Idara ya Uhamiaji ilifanya utafiti wa watalii wanaondoka nchini kwa lengo la kupata taarifa zitakazosaidia kuandaa akaunti za taifa na takwimu za mizania ya malipo ya nje; uandaaji wa mipango na sera; pamoja na utangazaji utalii.

Utafiti huu ulifanyika katika vituo vikubwa nane (8) vya kuingilia wageni vya viwanja vya ndege vya Mwalimu Julius Nyerere, Kilimanjaro na Abeid Amani Karume na vituo vya mpakani vya Namanga, Manyovu, Tunduma, Horororo na Mutukula. Matokeo ya utafiti huu ni pamoja na:

i. Mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kwa asilimia 83 hadi kufikia Dola za Marekani 1,310.34 milioni kutoka Dola za Marekani 714.59 milioni zilizopatikana mwaka 2020.
ii. Masoko makubwa 15 yalichangia asilimia 81 ya watalii wote ikilinganishwa na asilimia 71.8 mwaka 2020.  Masoko hayo yaliongozwa na Ufaransa ambayo ilikuwa na asilimia 15.3 ikifuatiwa na Marekani, Kenya na Zambia.
iii. Wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliongezeka hadi Dola za Marekani 199 kutoka Dola za Marekani 152 mwaka 2020.
iv. Watalii waliokuja kwa ajili ya likizo na burudani walikuwa asilimia 59 na wameendelea kuwa na wastani mkubwa wa matumizi sawa na Dola za Marekani 350 kwa siku. Watalii walionunua huduma kwa vifurushi walitumia wastani wa Dola za Marekani 364.0 kwa siku na wale ambao hawakununua huduma na bidhaa kwa vifurushi walitumia wastani wa Dola za Marekani 141.0.

v. Watalii waliyotembelea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walikaa kwa wastani wa siku 10 sawa na mwaka 2020. Watalii wanaotoka nchi za mbali walikaa kwa siku nyingi zaidi ikilinganishwa na wale waliotoka nchi jirani
vi. Utalii wa wanyamapori umeendelea kuwa kitovu cha vivutio vya utalii nchini ukifuatiwa na utalii wa fukwe.  Kuwepo na hifadhi za wanyama na mapori ya akiba mengi pamoja na fukwe zenye mandhari nzuri kumefanya utalii wa wanyamapori na fukwe kuendelea kushamiri hapa nchini..
Matokeo ya utafiti huu yatasaidia kuandaa mikakati ya kukuza na kuendeleza utalii apa nchini.  Aidha, wdau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi ambayo ni kiini cha kukuza utalii watatumia matokeo haya katika mipango yao ya kuimarisha huduma wanazozitoa.
Taarifa ya utafiti huu inapatikana kwenye tovuti zifutazo: www.maliasili.go.tz, www.bot.go.tz, www.zanzibartourism.net, www.nbs.go.tz na www.moha.go.tz

                  ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

 

© 2022 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top