You Are Here: Home » Whats New » TAARIFA KWA UMMA - MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO 19

TAARIFA KWA UMMA - MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO 19

TAARIFA KWA UMMA - MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO 19

Wizara ya Maliasili na Utalii ni moja ya wanufaika wa mkopo huu na imeidhinishiwa kiasi cha Shilingi 90,202,345,530 ambayo ni sawa na asilimia 6.9 ya fedha yote iliyotengwa kutekeleza majukumu mbalimbali ndani ya mwaka wa fedha 2021/2022. Katika utekelezaji huo, Wizara ya Maliasili na Utalii itajikita katika maeneo matano (5) ambayo yameathirika zaidi kutokana na Ugonjwa wa UVIKO-19. Ni matumaini ya Wizara na Serikali kwa ujumla kuwa utekelezaji huu utasaidia kuinua utalii na kuifanya sekta hiyo kuendelea kuchangia katika uchumi na maendeleo ya nchi. Furaha ya Serikali yetu ni kuna wadau wa utalii pamoja na wananchi kwa ujumla wanaendelea kufanya kwa ufanisi shughuli za utalii pamoja na uwepo wa Janga la UVIKO-19.

Maeneo ya utekelezaji ni kama ifuatavyo:

1. Kuziwezesha Taasisi za Wizara zilizoathirika zaidi kutokana na Mlipuko wa UVIKO-19 (TANAPA, TAWA, NCAA, TFS na NMT) kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Kiasi cha TZS.71, 904,345,530 zimetengwa na mchanganuo ni kama ifuatavyo:- i. Kukarabati barabara zenye urefu wa kilomita 4,881 katika maeneo ya hifadhi (Serengeti, Katavi, Mkomazi, Tarangire, Nyerere, Kilimanjaro, Saadani na Gombe, Eneo la hifadhi ya Ngorongoro , Misitu kumi (10) ya hifadhi ya mazingira asilia chini ya TFS) ambazo zitagharimu Shilingi Bilioni 23,400,000,000.

Kama mnavyojua maeneo mengi ya utalii kwa kutotembelewa kwa muda mrefu na watalii, miundombinu mingi imeharibika na hivyo inahitaji kukarabatiwa tena ili iweze kuendelea kutumika. Hivyo, hatua hii itasaidia kufikika kwa urahisi kwa vivutio vya utalii na kukidhi kiu ya watalii na hivyo kuchochea shughuli za utalii ambazo kwa sasa zimetetereka kwa kiasi kikubwa kutokana na janga la UVIKO – 19.

ii. Kuweka mifumo ya kielektroniki (Develop eletronic tracking systems) ya ufuatiliaji wa mashine kubwa na magari katika taasisi za uhifadhi. Jumla ya TZS. 1,000,000,000 zimetengwa. iii. kukarabati viwanja vya ndege nane (8) katika hifadhi za Taifa za: Serengeti, Nyerere,Tarangire, Mkomazi, Saadani na Katavi. Katika kufanikisha kazi hizo jumla TZS. 3,000,000,000 zitatumika.

iv. Kujenga malango matano (5) ya kupokelea wageni katika maeneo ya Likuyu Sekamaganga na Msolwa katika hifadhi ya Nyerere, hifadhi ya Mkomazi, Mapori ya Akiba ya Swagaswaga na Kijereshi. Kila lango litajumuisha maegesho ya magari, ofisi, maliwato (public toilets), mtandao wa maji ambao utahusisha uchimbaji wa kisima na mitambo ya umeme wa jua, ujenzi wa nyumba za watumishi, miundombinu ya TEHAMA ya kukusanya mapato, ununuzi na magari matatu (3). Kazi hii itagharimu TZS. 10,200,000,000.

v. Kununua jumla ya seti 5 za mitambo ili kuwezesha ujenzi na ukarabati miundombinu katika hifadhi kumi na tatu (13) za Taifa za: Serengeti, Ziwa Manyara, Mkomazi, Arusha na Kilimanjaro, Burigi-Chato, Ibanda-Kyerwa, Rumanyika-Karagwe, Kigosi na Rubondo na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Tarangire na Nyerere ambapo Jumla ya TZS 21,226,291,391 zimetengwa.

vi. Kununua boti maalum yenye kioo kwa ajili ya utalii wa baharini itakayotumika katika eneo la Kilwa Kisiwani itakayo itagharimu jumla ya TZS.500,000,000. Hatua hii pamoja na manufaa mengine, itawezesha kupanua wigo wa vivutio vya utalii katika maeneo ya kusini na kuimarisha utalii wa fukwe nchini. vii. kukarabati miundombinu ya utalii ikiwemo barabara na vituo vya taarifa za watalii katika mapori ya akiba 11 na mapori tengefu sita (6) kwa ajili ya kuendeleza utalii wa picha. Wizara inategemea kutumia kiasi cha TZS.8,500,000,000;

viii. kununua seti za mitambo ya kujenga na kukarabati miundombinu katika maeneo ya pori tengefu la Kilombero na mapori ya akiba ya Mkungunero na Moyowosi. Mitambo hii itahusisha ununuzi wa gari moja la kuchimba visima, Kununua boti maalum (Amphibous boat) ya kufanya doria kwenye maeneo chepechepe/ardhioevu na mashine za kuchimba visima. Gharama za matumizi hayo ni TZS. 2,178,054,139; ix. Kuimarisha udhibiti wa ubora wa huduma za utalii katika kukabiliana na janga la UVIKO-19 kwa:-

i. Kuweka mifumo ya kielektroniki ya kutambua, kuhakiki na kupanga huduma za malazi katika daraja za ubora; ii. Kutoa mafunzo kwa wataalamu wa tathmini (Assessors), wakufunzi, walimu wa wakufunzi, na watoa huduma za malazi katika kupanga daraja za ubora ; iii. Kuboresha miundombinu ya mifumo ya kielektroniki ya kukusanya mapato inayowezeshwa na mkongo wa Taifa wa mtandao wa TTCL;

iv. Kununua mifumo (software) kwa ajili ya miundombinu ya TEHAMA; v. Ununuzi wa magari matatu (3) kwa ajili ya kazi za udhibiti wa ubora na kujenga uelewa wa miongozo (SOPs) mbalimbali ya udhibiti wa UVIKO-19. Jumla ya kiasi cha TZS.1,900,000,000 zitatumika katika kutekeleza shughuli hizo.

Ndugu Wanahabari, Eneo la pili ambalo fedha hizi zitaelekezwa ni kuimarisha masoko na kutangaza utalii. Kiasi cha TZS 13,318,000,000 zimetengwa na mchanganuo ni kama ifuatavyo: Katika eneo hili shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na :-

(i) Kukarabati vituo saba (7) vya Urithi wa Kiutamaduni vya Mikindani Mtwara,Tendaguru-Lindi, Magofu ya Kua-Mafia, Msikiti wa Mbua Maji Mbweni, Makaburi na Msikiti wa bandarini na Kimbiji- Dar es Salaam. Jumla ya TZS 2,450,000,000 zitatumika. ii) Ujenzi wa kituo cha kutolea taarifa za utalii katika hifadhi ya Taifa Burigi-Chato katika Lango la Meja Jenerali Kijuu. Jumla ya TZS 300,000,000 kitatumika.

iii) Kununua vifaa kwa ajili ya kituo cha kutolea taarifa za utalii kidigitali ili kuwezesha utangazaji wa utalii kwa kutumia mitandao ya kijamii na tovuti (Digital Command Center) pamoja na gharama za kulipia mfumo wa kutangaza vivutio vya utalii kidigitali. Jumla ya TZS 568,000,000 zitatumika.

iv) Kutanua wigo wa programu ya The Royal Tour kwa:- kukusanya taarifa mbalimbali za utalii katika maeneo mahsusi ya hifadhi, vivutio vya utalii Tanzania bara na Zanzibar na kuweka mikakati ya kuvitangaza ndani na nje ya nchi. Aidha, programu hii itajumuisha gharama za kuandaa na kurusha vipindi na kulipia matangazo mbalimbali nje ya nchi hususan katika vyombo vya habari vya kimataifa kwa kuhusisha watu maarufu duniani ili kuitangaza nchi yetu zaidi. Jumla ya TZS 6,000,000,000 zitatumika.

v) Kuwezesha maonesho mawili (2) ya kimataifa. Jumla ya kiasi cha TZS. 4,000,000,000 kitatumika. Ndugu Wanahabari, Eneo la tatu ambalo fedha hizi zitatumika ni kuimarisha mazingira ya biashara ya Utalii kwa kuzingatia viwango vya afya na usalama vya kitaifa na kimataifa. Kiasi cha TZS 1,800,000,000 zimetengwa na mchanganuo ni kama ifuatavyo: Katika eneo hili shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na :- Kuimarisha upatikanaji wa chanjo na vifaa vya upimaji wa UVIKO-19 katika sekta ya utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya TAMISEMI kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya. Aidha, Wizara itajenga uelewa miongoni mwa wafanyabiashara wa utalii juu ya miongozo ya kukabiliana na Janga la UVIKO-19 katika mikoa 26 nchini. Jumla ya kiasi cha TZS. 1,800,000,000 zitatumika.

Ndugu Wanahabari, Eneo la nne ambalo fedha hizi zitatumika ni kushirikisha Sekta Binafsi kwa kuwajengea uwezo wa kukabiliana na janga la UVIKO-19. Kiasi cha TZS 1,380,000,000 zimetengwa. Katika eneo hili shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na :-

i. Kununua na kusambaza vifaa kwa wadau wa sekta ya utalii kwa ajili ya kujikinga na janga la UVIKO-19 na kutoa mafunzo juu ya namna ya kutumia vifaa tiba husika. Shughuli hii itagharimu kiasi cha TZS.1,200,000,000.

ii. Kutoa mafunzo na mikakati mbalimbali kwa wadau wa sekta ya utalii katika mikoa iliyoathirika zaidi ikiwemo Mtwara, Ruvuma and Lindi, Njombe, Mbeya, Mara na Mwanza. Kazi hizi itagharimu kiasi cha TZS. 180,000,000. Ndugu Wanahabari, Eneo la tano ambalo tutalipa kipaumbele ni kuimarisha mifumo ya kidigitali ya takwimu za utalii. Katika eneo hili shughuli itakayotekelezwa ni kuboresha mifumo ya taarifa na takwimu za watalii kwa kufanya utafiti wa matumizi ya shughuli za utalii kwa kaya ili kubaini mchango wa sekta ya utalii katika Pato la Taifa. Kazi hii itagharimu kiasi cha Jumla ya TZS.1,800,000,000. Kwa ujumla Wizara imetengewa kutumia jumla ya Shilingi 90,202,345,530 katika kutekeleza maeneo hayo matano katika mpango huu.

HITIMISHO

Napenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha hizi ambazo zimepatikana katika muda muafaka kuokoa sekta ya utalii ambayo imeathiriwa zaidi na Janga la UVIKO-19. Niwahakikishie Watanzania kwamba Wizara imejipanga vyema kuhakikisha mipango yote hii itakamilika na kutekelezwa ndani ya mwaka huu wa fedha 2021/2022 ili kuifanya sekta ya utalii iendelee kuchangia katika pato la Taifa na maisha ya wananchi kwa ujumla. Lengo pia ni kuendelea kuitekeleza kaulimbiu yetu kwa vitendo ambayo inabainisha kuwa: TUMERITHISHWA, TUWARITHISHE. PAMOJA NA UVIKO-19, KAZI IENDELEE

Asanteni kwa kunisikiliza

Dkt. Damas D. Ndumbaro (Mb.)

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII

17 Oktoba, 2021

TAARIFA_KWA_UMMA_KUHUSU_UTEKELEZAJI_WA_MPANGO_WA_MAENDELEO_KWA_USTAWI_WA_TAIFA_NA_MAPAMBANO_DHIDI_YA_UVIKO_%E2%80%93_19_KATIKA_SEKTA_YA_MALIASILI_NA_UTALII_%28FEDHA_ZA_MSAADA_KUTOKA_SHIRIKA_LA_FEDHA_DUNIANI_-_IMF%29_%282%29

© 2022 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top