You Are Here: Home » Whats New » Serikali Yakanusha Kuhusu Utoroshaji wa Wanyamapori Katika Pori la Loliondo

Serikali Yakanusha Kuhusu Utoroshaji wa Wanyamapori Katika Pori la Loliondo

Serikali Yakanusha Kuhusu Utoroshaji wa Wanyamapori Katika Pori la Loliondo

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekanusha uzushi uliosambaa kwenye Mitandao ya Kijamii kuhusu utoroshwaji wa nyara za Taifa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mpingo House, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Adelhelm Meru, amesema hakuna twiga yoyote wala nyara ya aina yoyote iliyosafirishwa kupelekwa nje ya nchi.

Dkt. Meru ameelezea kusikitishwa kwake na picha za kughushi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinalenga kuchafua taswira ya Taifa.
Dkt Meru amesema picha zinazosambazwa zimechukuliwa kutoka kwenye mitandao na kuelezewa kama ni za hapa nchini.
Akikanusha uzushi huo Dkt. Meru amesema, kupitia Kampuni ya Kitalii ya Ortello Business Corporation Ltd ambao ni wamiliki wa kitalu hicho katika Pori tengefu la Loliondo, ilikuwa na ugeni kutoka Falme za Kiarabu akiwemo Mfalme wa Dubai Bw, Sheikh H.H. Mohamed Bin Rashid na Waziri Mkuu wa Falme za Kiarab.

Dkt. Meru amesema wageni hao walipewa vibali vya kuwinda ambavyo vililipiwa kiasi cha dola 41,400 za Kimarekani wakiruhusiwa kuwinda wanyama akiwemo fisi, swala, pofu na aina mbalimbali za ndege. 
Dkt. Meru amebainisha kuwa uwindaji huo ulifanyika kwa siku nne ambapo mnamo tarehe 24 mwezi huu , zilikuja ndege tatu, mbili zikiwa zimebeba watumishi, wageni wawindaji, wageni watazamaji, walinzi wa mfalme huyo, Waziri wa Falme za Kiarabu pamoja na Mfalme wa Dubai jumla yao walikuwa 137 na ndege ya tatu ilikuwa imebeba mizigo pamoja na vifaa vya uwindaji.
Aidha , Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii aliweka bayana kuwa wawindaji hao wa kitalii wakati wanafanya shughuli hizo waliambatana na maafisa kutoka Jeshi la polisi,  Usalama wa Taifa pamoja na maofisa kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili ( KDU) kilichopo Arusha,PICHANI: Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Adelhelm Meru,akizungumza na waandishi wa habari leo ( hawapo pichani kuhusu ) Mpingo House jijini Dar es Salaam,  kuhusu uzushi uliosambaa kwenye Mitandao ya Kijamii kuhusu ndege na wazungu walionekana kwenye picha wakiwa na twiga kuwa ni picha zakugushi na pia   hazina ukweli wowote. Wengine katika picha ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Bw.  Herman Keryaro ( wa kwanza kushoto) akiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori,  Dkt. Mulokozi na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Dorina Makaya.

Mfalme wa Dubai, Bw, Sheikh H.H. Mohamed Bin Rashid na Waziri Mkuu wa Falme za Kiarabu na msafara wake walitua katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro tarehe 24 mwezi Septemba 2015, walifanya uwindaji kwa muda wa siku nne na kuondoka hapa nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kilimanjaro tarehe 29 Mwezi Septemba. Hawakusafirisha nyara yoyote.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Adelhelm Meru, amesema, Uwindaji wa Kitalii pamoja na usafirishaji wanyamapori kwa mujibu wa sheria ya wanyamapori ni kitu cha kawaida kabisa endapo taratibu zote zinafuatwa.

Taratibu hizo ni pamoja na kupata kibali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii. Dkt. Meru ameeleza bayana kuwa, uwindaji unafanyika nchi mbalimbali duniani lengo likiwa ni kupunguza madhara yanayoweza kutokea kwa binadamu endapo wanyama watakuwa wengi zaidi pamoja na nchi kupata mapato yatokanayo na uwindaji huo.

© 2022 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top