You Are Here: Home » Whats New » ONGEZENI KASI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UVIKO 19.

ONGEZENI KASI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UVIKO 19.

Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zimetakiwa kuongeza kasi katika Utekelezaji wa miradi yote inayo tekelezwa na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa kuzingatia ubora kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa.

Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (MB) alipokuwa akipokea taarifa ya Utekelezaji wa mpango huo katika Sekta ya Maliasili na Utalii.

Mhe. Chana amesema kukamilika mapema kwa miradi yote chini ya mpango huo kutasaidia kuongeza watalii wa ndani na nje kwenye maeneo ya vivutio vya Utalii na kuiongezea Serikali Mapato.

Akitoka taarifa ya Utekelezaji wa Miradi hiyo ya UVIKO 19 ndani ya Wizara, Mratibu Mkuu wa Miradi hiyo ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Bw. Boniface Malya amesema licha ya changamoto chache zilizopo wameweza kukabiliana nazo kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli zilizobaki ili miradi hiyo ikamilike kwa muda uliopangwa, kuongeza kasi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mvua inapopungua na kuwafuatilia kwa karibu wakandarasi ili wakamilishe miradi kwa wakati.

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Mary Masanja (MB), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Francis Michael, Mkurugenzi wa Idara Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Prisca Lwangili, Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara pamoja na Viongozi wa Taasisi za Wizara.

© 2022 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top