You Are Here: Home » Whats New » NAIBU WAZIRI KANYASU AWATAKA TFS KUTUMIA BODABODA KUKABILIANA NA WASAFIRISHAJI MKAA

NAIBU WAZIRI KANYASU AWATAKA TFS KUTUMIA BODABODA KUKABILIANA NA WASAFIRISHAJI MKAA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewataka Watendaji wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) waanze msako kwa kutumia Bodaboda (Pikipiki) ikiwa ni mbinu mpya ya kukabiliana na wananchi wanaosafirisha mazao ya misitu kwa kutumia baiskeli na pikipiki.

 

Amesema watumiaji wa vyombo hivyo wamekuwa wakikwepa kulipa kodi na tozo stahiki na hivyo kuisababishia serikali kupoteza mapato yake.

Mhe. Kanyasu ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati akifungua kikao maalumu cha utendaji ambacho kimewakutanisha pamoja viongozi wa TFS kuanzia makao makuu hadi katika ngazi ya wilaya


“Anzeni kufanya doria kwa kutumia pikipiki kama ilivyo kwa Jeshi la polisi linavyotumia pikipiki kuwanasa baadhi ya watuhumiwa” Alisisitiza Kanyasu.


Akizungumza katika mkutano huo, Mhe.Kanyasu amesema pikipiki na baiskeli zimekuwa zikisafirisha magunia ya mkaa ambayo ni mengi yanayoweza kusafirishwa na lori.


Katika mkutano huo, Mhe.Kanyasu amewaonya watendaji hao waache kutumia vizuizi ikiwa pamoja na kufunga kamba barabarani kwa ajili ya kuwakamata waendesha pikipiki na baiskeli waliobeba mkaa hali inayopelekea wahalifu kuanguka na kuumia wakati wakijaribu kukimbia ili wasikamatwe

Badala yake amewataka Watendaji hao watumie pikipiki katika kupambana nao ili kuwaepusha na madhara wanayoweza kuyapata watuhumiwa hao endapo watatumia vizuizi barabarani.

“Ninyi mmepitia mafunzo ya Jeshi USU ni lazima muende sambamba na njia wanazozitumia wahalifu,anzeni kutumia Bodaboda kama wao wanavyotumia ” alisisitiza Kanyasu


Ameongeza kuwa usafirishaji huo kwa njia ya pikipiki na Baiskeli lazima udhibitiwe kwa kutumia mbinu rafiki za kuwanasa bila kuwasababishia madhara waendeshaji wa vyombo hivyo.

Aidha, Mhe.Kanyasu ametoa onyo kwa wasafirishaji mkaa wanaotumia pikipiki na baiskeli kuwa waache mara moja la sivyo hawatasalimika.

Kwa mujibu wa mwongozo wa uvunaji endelevu wa mazao ya misitu ya asili wa mwaka 2015, vyombo vinavyoruhusiwa kusafirisha mazao hayo ni vyenye magurudumu manne

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewataka Watendaji wa TFS waelekeze nguvu zao zaidi katika kuzuia miti isikatwe badala ya kukimbizana na wasafirishaji wa mazao ya misitu ikiwa tayari mazao yapo barabarani.


” Nawakumbusha kazi yenu ya msingi ni kulinda misitu isiharibiwe na sio kuacha misitu iharibiwe ndipo muanze kukimbizana na wasafirishaji haramu huko barabarani”

Ameongeza kuwa katika jamii kumekuwa na hisia kuwa kukata miti sio kosa ila linakuwa kosa pale unaposafirisha.

Mhe.Kanyasu amesema pikipiki na baiskeli vimechochea kwa kiasi kikubwa uharibifu wa misitu ambapo kwa mujibu wa taarifa zinaonesha kuwa mkaa husababisha upotevu wa wastani wa hekta 372,000 za misitu kila mwaka.

Amesema uvunaji huo hupoteza walau asilimia 1.1 ya eneo lote la misitu nchini.

 

 

© 2020 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top