You Are Here: Home » Whats New » MHE.KANYASU ATAKA MAMENEJA WA MAPORI NCHINI KUHIFADHI KIBIASHARA

MHE.KANYASU ATAKA MAMENEJA WA MAPORI NCHINI KUHIFADHI KIBIASHARA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewataka Mameneja wanaosimamia Mapori ya Akiba na Hifadhi za Mazingira Asilia nchini waanze kufikiri kibiashara kulingana na shughuli wanazozifanya badala ya kujikita kuhifadhi kwa ajili ya Bioanuwai pekee.

Hayo ameyasema leo wakati alipotembelea maonesho ya NaneNane yanayoendelea kufanyika kwa muda wa siku tatu zaidi mara baada ya jana kufikia kilele chake katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Amesema katika Hifadhi hizo kuna misitu yenye utajiri mkubwa wa kuwawezesha kufungua mashamba maalum ya nyuki ili kukidhi mahitaji ya soko ya asali katika nchi ya China ambapo hata nusu ya mahitaji hayajafikiwa ya inahitajika nchini humo.


Amesema mbali ya kufungua mashamba hayo ya nyuki bado kuna fursa lukuki za kuanzisha utalii wa picha ambapo watalii wa kutoka nje na ndani ya nchi watafika kwa ajili kujionea wanyamapori pamoja na kufanya tafiti mbalimbali za kisayansi katika Hifadhi hizo.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Kanyasu amewataka wabuni shughuli mbambali zitakazokuwa zikifanyika katika Hifadhi hizo zitakazoweza kuwaingizia kipato pasipo kuathiri hali ya Uhifadhi.

” Kazi yenu kubwa ni kufikiria usiku na mchana kuona namna ya kufanya biashara kupitia Hifadhi mnazozisimamia” Alisisitiza Kanyasu


Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewataka Mameneja hao wasifanye kazi kwa mazoea badala yake waje na mawazo mapya ya namna ya kuongeza mapato katika mapori na Hifadhi hizo wanazozisimamia.

” Katika dunia ya sasa huwezi ukawa unafanya kazi moja tu ya kuhifadhi bila kujua mwisho wa siku unapata nini, Ninawataka mbadilike hifadhini kimkakati” alisema Kanyasu.

Amesema hata ikiwezekana watengeneze sehemu ya kuonea wanyama kwa kuchimba mabwawa ambapo maji yake yatakuwa hayakauki muda wote hali itakayowafanya wanyama kukusanyika katika maeneo hayo kwa ajili ya kunywa maji hayo.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewataka Mameneja hao kuja na mkakati wa kuvitangaza vivutio hivyo watakavyovibuni kwa vile watalii wote wanaotembelea vivutio vilivyopo nchini nyuma yake kuna kazi kubwa imefanyika.“Kuna na vivutio ni jambo na kuvitangaza ni jambo jingine” Amesisitiza

 

© 2020 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top