You Are Here: Home » Whats New » Mchango wa Uhifadhi Katika Kukuza Uchumi wa Nchi na Umuhimu wa Wananchi Kushiriki Kuzuia Ujangili

Mchango wa Uhifadhi Katika Kukuza Uchumi wa Nchi na Umuhimu wa Wananchi Kushiriki Kuzuia Ujangili

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Wanyamapori ina dhamana ya kuhifadhi rasilimali ya wanyamapori nchini. Ili kutekeleza uhifadhi huo, Tanzania imetenga maeneo ya uhifadhi yenye ukubwa wa takriban asilimia 28 ya nchi kavu ya Tanzania Bara. Maeneo hayo yanajumuisha; Hifadhi za Taifa 16, Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, Mapori ya Akiba (Game Reserves) 28, Mapori Tengefu (Game controlled Areas) 44 na Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (Wildlife Management Areas) 38

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

 

TAARIFA KWA UMMA

MCHANGO WA UHIFADHI KATIKA KUKUZA UCHUMI WA NCHI NA UMUHIMU WA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA KUZUIA UJANGILI.

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Wanyamapori ina dhamana ya kuhifadhi rasilimali ya wanyamapori nchini. Ili kutekeleza uhifadhi huo, Tanzania imetenga maeneo ya uhifadhi yenye ukubwa wa takriban asilimia 28 ya nchi kavu ya Tanzania Bara. Maeneo hayo yanajumuisha; Hifadhi za Taifa 16, Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, Mapori ya Akiba (Game Reserves) 28, Mapori Tengefu (Game controlled Areas) 44 na Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (Wildlife Management Areas) 38.

Hapa nchini, kwa zaidi ya asilimia 90 utalii unategemea wanyamapori. Watalii wengi huja kuwaona tu wanyama, kuwapiga picha na kuondoka. Wachache huja kuwawinda kisheria na kuchukua nyara. Wanyamapori ndio wamebeba utalii katika Tanzania na kwa maana hiyo ndio, kwa kiasi kikubwa, wamebeba uchumi wa nchi hii – ndio wanatununulia dawa, vitabu mashuleni, wanatujengea barabara na, kwa watumishi wa umma, ndio wanatulipa mishahara.

 Wizara inatoa wito kwa Watanzania kuwa tuache kumtazama fisi kama mnyama mwenye sura mbaya na anayenuka; na tuache kumtazama tembo kama kero kwa wakulima na kwa hiyo kufurahia kuuawa kwao. Badala yake tuwatazame wanyamapori kama benki kubwa na kama mkombozi wa nchi yetu kiuchumi.

 Wanyamapori kama ilivyo kwa viumbe hai, huzaliana. Hivyo, kama tutashirikiana kuwalinda na kuwatumia kiendelevu si miaka mingi tangu sasa watakuwa namba moja katika kuchangia pato la Taifa letu.

 Kwa kipindi kirefu sasa vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, vimekuwa vikiripoti kuongezeka kwa ujangili nchini na, kwa hivi karibuni, zaidi mauaji ya kinyama ya tembo na usafirishaji haramu wa wanyamahai na meno ya tembo. Sekta ya wanyamapori inajitahidi sana kupambana na uhalifu huu kulingana na watumishi waliopo na fedha na vitendea kazi vilivyopo. Kwa mfano, mwaka 2012/13 pekee (kufikia Machi 2013) watuhumiwa 1,215 walikamatwa kwa makosa mbalimbali wakiwa na jumla ya bunduki 85 na risasi 215 za aina mbalimbali. Kesi 670 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini. Kati ya hizo, kesi 272 zimemalizika kwa washitakiwa 247 kulipa faini ya jumla ya shilingi 175,002,420/= na washitakiwa 71 kupewa adhabu ya vifungo vya jumla ya miaka 99. Aidha, kesi 398 zenye jumla ya washitakiwa 897 bado zinaendelea katika mahakama mbalimbali nchini.

 Kwa bahati mbaya, baadhi ya Watanzania wanaamini kuwa jukumu la kuzuia ujangili ni la serikali pekee na hasa maafisa na askari wanyamapori (walioko Idara ya Wanyamapori, TANAPA na Ngorongoro). Dhana hii ni potofu kabisa kwani, uzuiaji ujangili kamwe hautafanikiwa kama wananchi na wadau wengine walioko ndani na nje ya nchi yetu wataendelea kubakia watazamaji tu.

 Tuitafakari na kuitekeleza dhana ya Jeshi la Polisi ya Ulinzi Shirikishi. Ni muhimu kila mwananchi mzalendo wa nchi hii ashiriki kikamilifu kudumisha amani na ulinzi wa nchi na rasilimali zake zote. Hivyo basi, wananchi wanaweza kusaidia kupambana na ujangili kwa kutoa taarifa za kina na uhakika zitakazopelekea kukamatwa majangili na/au wafadhili wao. Yeyote mwenye taarifa azitoe ama kwa Afisa Wanyamapori aliye karibu yake, Makao Makuu ya Idara ya Wanyamapori, TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro au Kituo cha Polisi kilichokaribu.

 Kufuatia mawasiliano yetu na umma kwa njia ya vyombo vya habari, hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la watoa taarifa za ujangili. Baadhi ya taarifa hizo zimewezesha kukamatwa kwa baadhi majangili, nyara na silaha. Tunawashukuru sana waliotufikishia taarifa hizo kwa wakati na tunawaomba waendelee kutupa ushirikiano. Tanzania bila ujangili inawezekana - “Change ni mimi na wewe”. Hakuna mali ya serikali, ni wewe na mimi ninaoibiwa.

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.

Unaweza kupiga simu kwenye namba zifuatazo: 0754877019; 0787491600; 0713350405; 0784483599; 0754756585 au tuma barua pepe kwenda dw@mnrt.go.tz au ps@mnrt.go.tz

© 2021 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top