You Are Here: Home » Whats New » KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAISHAURI WIZARA KUHUSU TAFORI

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAISHAURI WIZARA KUHUSU TAFORI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeishauri Wizara ya Maliasili na Utalii kuiongezea fedha Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) ili iweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi na kupanua wigo wa huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

 


Ushauri huo umetolewa kwa nyakati tofauti na Wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Jijini Dodoma mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt.Revocatus Mshumbushi kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.

Akizungumza kwenye kikao hicho mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Zanzibar,  Mhe. Soud Jumah amesema TAFORI ni taasisi muhimu kwa mustakabali wa misitu nchini hivyo ni lazima iangaliwe ili iweze kufanya utafiti wa magonjwa ya miti pamoja na mbegu bora za miti

” TAFORI ni injini ni lazima iwezeshwe ili iweze kufanya utafiti pamoja na kuandaa maandiko yatakayosaidia wakulima wa miti hapa nchini kuzalisha mazao ya misitu yatakayokidhi viwango vya ubora vya ndani na nje nchi, amesema Mjumbe wa Kamati hiyo,Mhe Soud Juma
.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Flatei Massey ameshauri taasisi hiyo kujenga uwezo kwa kuwa na vitendea kazi yakiwemo magari ili kuwawezesha watalaam wa utafiti kusafiri maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya tafiti.

Naye,  Mhe.Jaffari Chege ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo na Mbunge wa Rorya ameitaka TAFORI kufanya utafiti wa kina na kutangaza matokeo ya utafiti huo kuhusu miti gani mbadala wa mbao ngumu ya mninga ili kuwasaidia wananchi kutumia mbao mbadala katika ujenzi wa nyumba zao

” Nawaalika kule jimboni kwangu Rorya mfanye utafiti miti gani mbadala ya mbao inayoweza kustawi ili tuweze kulima ” amesema Mhe. Chege

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Balozi Dkt. Pindi Chana amewahakikishia Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Wizara yake itaendelea kuisaidia Taasisi hiyo kadri fedha zitakavyokuwa zikipatika

‘‘Mimi kama Waziri mwenye dhamana natambua umuhimu wa Taasisi hii naomba niwakikishie kuwa tutazidi kuiangalia kwa karibu Taasisi hii kwani ndio dira yetu ya misitu hapa nchini ikizingatiwa kwa sasa tumewaongezewa jukumu lingine la sekta ya nyuki’’ amesisitiza Balozi Dkt. Pindi Chana.


Ameeleza kuwa kwa sasa Taasisi hiyo mbali ya kufanya tafiti za misitu imekuwa pia ikifanya tafiti za nyuki, jukumu ambalo hapo awali lilikuwa likifanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI)

 

© 2022 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top