You Are Here: Home » Whats New » DKT. NDUMBARO AONGOZA MAPOKEZI YA MUANDAAJI MAARUFU WA FILAMU ZA UTALII DUNIANI KUTOKA MAREKANI 

DKT. NDUMBARO AONGOZA MAPOKEZI YA MUANDAAJI MAARUFU WA FILAMU ZA UTALII DUNIANI KUTOKA MAREKANI 

DKT. NDUMBARO AONGOZA MAPOKEZI YA MUANDAAJI MAARUFU WA FILAMU ZA UTALII DUNIANI KUTOKA MAREKANI 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro leo Jumapili tarehe 27 Disemba 2020  aongoza mapokezi ya kumpokea Muandaaji maarufu wa taarifa na makala za utalii duniani, Drew Binsky katika Uwanja wa ndege wa  Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea nchini Marekani

 
Bw. Drew ni miongoni wa Waandaaji maarufu wa filamu za utalii mwenye wafuasi zaidi ya milioni 30 kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo facebook, instagram, snapchat, youtube pamoja na  twitter

Katika ziara hiyo,  Binsky  ameongozana na Mchumba wake, Deanne Visperas na  anatarajia  kutembelea Hifadhi za Serengeti na Ngorongoro na kumalizia ziara yake katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ambapo anapanga kupanda  Mlima huo katika siku za baadaye.

Akizungumza mara baada ya kumpokea,  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amemueleza kuwa Tanzania imekuwa kinara katika kufungua milango kwa wageni baada ya juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali na sekta binafsi katika kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa korona.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania na kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya utalii ndani na nje ya nchi  imeendelea kutumia mbinu mbalimbali kujenga imani kwa wageni kuwa Tanzania iko salama na ndiyo kituo bora zaidi cha utalii katika bara la Afrika.

Akizungumzia miongoni mwa hatua zilizochukuliwa kwa sasa katika kutangaza vivutio vya utalii, Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania imekuwa ikitumia  watu maarufu na mashuhuri duniani ambao wana ushawishi mkubwa na kupitia kwao dunia itaweza kufahamu zaidi kuhusu Tanzania.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Ndumbaro amewashukuru Mabalozi wa hiari kwa kujitoa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini  huku akimpongeza  Balozi wa hiari wa Utalii Bw. Nick Reynolds (Maarufu kama Bongozozo)  pamoja na Wadau wa sekta binafsi katika tasnia ya utalii  kwa kufanikisha kuratibu ziara ya Muandaaji maarufu wa taarifa na makala za utalii duniani,  Drew Binsky.

Amesema ujio wake nchini Tanzania  utasaidia kutangaza zaidi  vivutio viliyopo nchini kwa vile   Drew Binsky ni mtu maarufu wenye ushawishi mkubwa  na  amekuwa akitumia mfumo wa video kuwasilisha ujumbe wake kupitia mitandao yake ya kijamii yenye  wafuasi zaidi ya milioni 30.

Amesisitiza kuwa video zake atakazotengeneza katika maeneo ya vivutio atakavyotembelea zitaweza  kuwafikia  watu zaidi ya bilioni moja  Duniani.


Kwa upande wake, Muandaaji maarufu wa taarifa na makala za utalii duniani,  Drew Binsky ameshukuru kwa mapokezi aliyoyapata huku akiahidi kuwa atatumia mitandao yake ya kijamii kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na pia atakuwa Balozi mzuri pindi atakaporejea nchini kwao


 


 


 

© 2021 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top